Sunday 22 April 2012

Michango ya HOJA


CCM waenda mikoani kuukana ufisadi

*Wapeleka ujumbe wa NEC mkoa kwa mkoa
*Nape asema watapambana hadi washinde

Na Edmund Mihale, Dodoma

CHAMA Cha Mpinduzi (CCM) kimeanza ziara mikoani kupeleka ujumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM kwa wanachama kuwa kimedhamiria kupambana na ufisadi ndani na nje ya chama hadi kishinde.

Katibu wa Itikadi na Uenezi, Bw. Nape Nnauye aliyasema hayo Makao Makuu ya chama hicho mjini Dodoma jana, wakati akitangaza ratiba ya mapokezi ya Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Wilson Mukama na Sekretarieti ya chama hicho mkoani hapa.

Alisema chama hicho kimeandaa ziara kwa ajili ya kufikisha ujumbe wa Halmashauri Kuu kwa wanachama wake kuanzia leo ambapo watafanya makutano katika Uwanja wa Nyerere Square na kesho Mkoani Morogoro.

Alisema kuwa mapokezi hayo yataendelea katika Mkoa wa Pwani Wilaya ya Kibaha ambapo yatapokelewa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete. Alisema kuwa siku hiyo hiyo yataendelea katika Mkoa Dar es Salaam na Aprili 17 mwaka huu yatakuwa Zanzibar.

"Tutapambana na ufisadi hadi tushinde," alisema Bw. Nnauye.

Alisema kuwa CCM haitavumilia kuona inachafuliwa na watu wachache na kuwataka wanachama waliohama kwa hasira kutokana na kashfa ya ufisadi kurudi kundini.

Alisema uamuzi uliofikiwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa utafanyiwa kazi.Alisema uamuzi wa kuwachukulia hatua wanaojihusisha na ufisadi uko pale pale, hivyo wasidhani kuwa chama kimeishia hapo. 

"Ndugu zangu Halmashauri Kuu iliamua kuwa tutapambana na ufisadi hadi tushinde, hivyo kama alivyozungumza mwenyekiti, wanaotuhumiwa wajiandae, tumefunga milango na madirisha yote, ili kuhakikisha tunashinda," alisema Bw. Nnauye.

 Maoni:

   Nape hiyo sio njia ya kuushinda ufisadi. ccm itashinda tu ufisadi ikiwaweka ndani mafisadi wote na kutaifisha mali zote walizofisadi

  • nyie mnaosema mpo mjini ndio maana shudia maandamano ya ccm ndio utajua kuwa wanapendwa na wananguvu kubwa kaeni pembeni nendene mboe club mkaombe kazi mtapewa tu
  • Ni ngumu CCM kushinda ufisadi kwani mwenyekiti haamini kama upo. Itakuwaje amnyanyue mkono Lowasa mbele ya watanzania kuwa ndiye mgombea anayefaa Monduli? Hata kama maakama hajasibitisha lakini ripoti ya mwakyembe si ameisoma na Lowasa alipewa nafasi hakukana mbele ya bunge.Ufisadi ni best fiend wa CCM huwezi kuwatenganisha.Dawa si kuzunguruka mikoani, bali kushughulikia vilivyo mafisadi watuhumiwa wote. CCM hamjashtuka tu!kuwa watanzania wanaelimika kwa kasi kuhusu siasa!
  • HAWAWEZI KUSHUGHULIKIA MAFSADI KWA KUZUNGUKA NCHI NZIMA. KWANI HIYO SI DHAMIRA YAO, NI HADI VYAMA VYA UPINZANI NA WANANCHI WAPIGE KELELE WE, NDO WAJUE KUWA KUNA MAFISADI NDANI YA CHAMA. NI MIAKA MINGAPI SASA KELELE HIZO ZIMEPIGWA. UNAONA WANAVYOKURUPUKA HATA JINSI YA KUPAMBANA NA UFISADI NDANI YA CHAMA, ETI KUZUNGUKA NCHI NZIMA KUWAELEZA WANANCHI. HEBU WAFUKUZENI KABISA UANACHAMA TUONE KAMA MNA NIA YA DHATI KWELI YA KUPINGA UFISADI.

  • nakuaminiya Nnauye ccm chama makini na ishallah mungu akipenda kitaendelea kushinda tu siku hadi siku hawa chadema chama cha kibaguzi tushakiishutukizia kazi yao kueneza chuki tu ila kwa uwezo wa mola tutashinda tu ubunge ,udiwani,Uraisi na katika chaguzi zote za kisiasa hawa ambao wanapiga kelele ni wehu tu na wahuni ila ccm chama makini na kitaendelea kutawala mpaka kiama hapa hatutoi nchi mtazunguruka nchi nzima mpaka mtoke majasho ya ulimi lakini ccm itashinda tu na itaendelea kutawala daimaWewe unayesema hamtoi nchi 


    unamaana gani? ni ya mjomba wako kwani? unadhani Bhagbo alipenda kuiachia hata nyie tutawalazimisha kama mkikiuka utaratibu.
    NAPE HUWEZII! UMEWEKWA HAPO CHAMBO TU.Wewe na wenzio mnao ubavu wa kuumaliza ufisadi?Jitahidi lakini chunga sana usije poteza moto.wenye pesa huwawezi.Ndio maana wazee wamekutanguliza wewe!
  • Nape atanusa kama paka likimshinda anajeza nduki. Yetu macho kama wenye damu ya CCM WAMESHINDWA SEMBUSE SISIMIZI.

    CCM haiwezi kumtoa Lowassa, Chenge na Rostam kwenye chama, kama hawaitakii mema CCM basi wajaribu waone! Msitudanganye kuwa mmejivua GAMBA hii ni kukimbia kivuli chako! Iweje Mafisadi wapewe Siku 90 za kupima waone kama wanafaa kuendelea au? Huu ni uhuni na uonevu mkubwa hasa viongozi wa chini maana wao wakifanya makosa kidogo tu,atakimbizwa kama kuku kwenye nafaka! Kama kweli mwenyekiti alikuwa na nia ya kuwaondoa kwenye uongozi hao watu ni siku ile ile angewambia wajiuzulu! Mbona secretariete haikupewa muda wa kupima wao wamepewa? Huu ni uonecu na inathibitisha kuwa chama chetu ni cha watu wachache tena wafanyabiashara wakubwa na sio wakulima na wafanyakazi kama ilivyo kuwa hapo mwanzo! Kama tunataka kupata imani kwa wananchi kuvunja secretariet pekee hakutoshi! Waondoke wale wote wasiokitakia mema chama na wamekifanya kikose dira kwa vijana walio wengi! (maana wazee (Makada) waliowengi wanazidi kupungua kila kukicha)!
  • Kingine kinachofanya chama kikose Mvuto kwa jamii ni kule kuendekeza ufamilia katika chama, eti kisa ni mtoto wa fulani basi apewe nafasi (Mfano Ridhiwan, Nnape, Makamba, mwinyi, Karume, na wengine) Najua wengine mtarukia hoja kuwa kama wanasifa wasipewe? Lah hasha! Wapewe kwa kufuata utaratibu kama wengine wanavyofuata sio kwa kutoa favor (Kwa kuwa baba au mama ake ni fulani...). Tukumbuke yanayotokea Misri Libya na kwingine yalianza hivi hivi na mwishoe tukaona viongozi wakitaka kuwasimika watoto wao nyadhifa fulani kama hali hii haita dhibitiwa katika chama basi tutegemee yaliyotokea Misri.

    jamani nasema tena CCM ni chama makini chama cha wasomi sio chama cha kihuni au cha kikabila kama chadema ccm ni chama cha watu ambao walokwenda shule sio chama cha kichaga au cha kihaya hichi sisi msimamo wetu ni maendeleo kwa wananchi na hatutosita kuleta maendeleo kwa kelele zenu mwenye macho hambiwi tazama nchi toka alipoondoka nyerere maendeleo mangapi yamepatikana mpaka sasa acheni kelele zenu hizo nyinyi chadema ni watu hatari kama sumu ni wabinafsi na niwatu wajanja ambao mnataka nchi ili muweze kuitumia kwa masilahi yenu nakwambieni kama mmechelewa sio leo tena CCM sio daladala kila moja akawachiwa abande tu leo aje huyu kesho huyu serekali hatutoi ngo
  • Rostam na Lowassa walishiriki kwa kiasi kikubwa sana kumweka Kikwete madarakani mwaka 2005. Haiwezekani akawatupa. Hii ni danganya toto. Haiwezekani Lowasa aliilazimisha Tanesco kuingia mkataba na Richmond/Dowans (ambayo Rostam ni mbia)bila Kikwete kujua.Mali ya kifisadi ya akina Rostam ilisaidia kumwingiza Kikwete ikulu; kwa hiyo atawatupa hadharani tu lakini ndani lazima awasidie. Kumbuka Kikwete alipochukua uenyekiti tu, alimfanya Rostam kuwa mweka hazina wa ccm.
  • CCM ni chama cha siasa. chama cha siasa kinawezaje kumpeleka mtuhumiwa mahakamani? hiyo ni kazi ya dola,,walaumiwe serikali na watu wake, maana hata watu wa Chadema wamo serikalini ndo mna wanaweza kusema uwongo na wasichukuliwe hatua.
  •            the GREEN planetApr 22, 2012 05:48 AM
  • Hii ndio CCM naamini ni Chama Cha Siasa na Si Chama Cha SI HASA.wanajua wanacho kifanya.Wanauzoefu wa kushughulikia WAKENGEUFU wa Malengo na IMANI ya chama chao ambao kwa sasa tunawaita MAFISADI. wakati wa chama kimoja walikuwepo pia lakini walishughulikiwa kwa OPERATION maalum kama Azimio La Arusha, Uhujumu wa Uchumi, Fagio la Chuma nk kwa kizazi kile.

    Kwa kizazi hiki cha watu waliojaa ujanjaujanja naamini wanawashughulikia kwa MTINDO maalum. Wakikurupuka tu,hao hao wanaoitwa MAFISADI watahamia kwao na kwa kuwa wamejaaliwa kuupepeta watawasafisha na kwa hakika watakuwa safi wao na mihela yao.

    Imani yangu kuwa MTINDO wa CCM wanaoutumia uko sahihi DELAYING TACTICS ili HAO,WEWE NA MIMI tuwasemeeeeeeeeee Tuwachafuweeeeee Tuwaumbueeeeee na kama ushahidi upo tuendelee kuwaanikaaaaaaaaaa
    wasifae kabisa kabisa si kwa CCM na Kwa WAO hapo lengo la CCM linakamilika bila KUIATHIRI. Halafu sasa mdogomdogo haooooooooooooooooooo

    Mambo ya Shule sio KUKOPI NA KUPESTI baba kuwa mpole HII NDO CCM

Saturday 21 April 2012



MKEREKETWA WA MAZINGIRA WILAYANI MEATU ALIYEIBUKA NA USHINDI WA UTUNZAJI MAZINGIRA KITAIFA - 2010.





FRIDAY, AUGUST 13, 2010


“JUNI 5, 2010 ni siku ambayo haitasahaulika kwangu, ni siku ambayo niliamini kuwa ule msemo wa mtu kulala masikini na asubuhi kuamka tajiri, ni usemi wenye ukweli, na unawatokea watu,”

“Ni siku ambayo kwa mara yangu ya kwanza niliandika historia katika nchi yetu baada ya kutangazwa kuwa ni mshindi katika shindano la utunzaji wa mazingira nchini, kwa kweli sikuamini masikio yangu pale nilipokuwa nimeketi,” ndivyo anavyoanza kueleza Bw. Mussa Nyamve Sambe mkazi wa kijiji cha Mwambengwa wilayani Meatu mkoani Shinyanga.

Bw. Sambe anasema alizaliwa katika kijiji cha Zebeya wilayani Maswa mkoani Shinyanga mwaka 1961 akiwa ni mtoto wa sita katika familia yao ya Mzee Nyamve Sambe ambapo mwaka 1974 alipelekwa shule na kuanza kusoma darasa la kwanza katika shule ya msingi Mwanyahina na kufanikiwa kumaliza darasa la saba mwaka 1980.

“Nilipomaliza darasa la saba sikufanikiwa kuendelea na masomo ya sekondari kutokana na uhaba wa shule za sekondari wakati huo ilikuwa ni vigumu sana kupata nafasi na hivyo nililazimika kubaki nyumbani nikisaidiana na wazazi wangu katika shughuli za kilimo,” anaeleza Bw. Sambe na kuongeza,

“Mwaka 1982 nilihamasika na suala la utunzaji wa mazingira ambapo pale nyumbani nilipanda miti miwili tu mmoja wa mpera na mwingine aina ya Mhi’gu, hii niliitunza mpaka ikakua vizuri na hapo nilihamasika zaidi na wazo la kuendelea kupanda miti mingi kadri nitakavyoweza ambapo mwaka uliofuata nilipanda miti 25, ikiwemo ya matunda na mingine ya asili,” anaeleza.

Anasema kutokana na kustawi kwa miti hiyo japo katika mwaka huo miti miwili ilikufa kutokana na kushambuliwa na wadudu, alipata hamasa zaidi na kuamua kutafuta eneo lake mwenyewe ambalo ataweza kupanda miti mingi kwa lengo la kutunza mazingira katika maeneo yao ya kijiji chao.

“Unafahamu eneo letu tulilokuwa tukiishi lilikuwa na ukame wa kutisha, lakini nilipochunguza nilibaini kuwa hali hiyo ilisababishwa na uharibifu wa mazingira uliofanywa na wazee wetu miaka ya nyuma wakidai kupambana na wadudu aina ya mbungo waliokuwa wakishambulia mifugo yao, hivyo walikata miti ovyo,” anaeleza Bw. Sambe.

Mkereketwa huyo wa mazingira anasema, alifanikiwa kupata eneo la ardhi lenye ukubwa wa ekari 80 kijijini lililokuwa halina miti ambalo hata hivyo katikati yake kunapita mto mkubwa uitwao mto Mwanhuzi, hivyo alianza shughuli za kuliandaa eneo hilo kwa ajili ya kupanda miti mbalimbali kwa lengo la kuligeuza kuwa eneo la hifadhi na la mfano katika kijiji chao.

“Nilipoanza shughuli za kupanda miti sikuwa na wazo kuwa ipo siku moja nitatembelewa na viongozi wa serikali ngazi ya wilaya, mkoa na kitaifa pia na watu wa aina mbalimbali kutoka taasisi zinazojishughulisha na utunzaji wa mazingira ili kuja kuangalia eneo hili, lakini leo hii nashangaa hata mawaziri wengi wa serikali wamenitembelea,” anaeleza.

Bw. Sambe anasema mwanzoni mwa mwaka 2010 aliweza kusikia tangazo redioni likiwataka wananchi ambao ni wakareketwa wa mazingira kushiriki katika shindano la Tuzo ya Rais juu ya utunzaji wa mazingira nchini, ambapo alihamasika na kuamua kushiriki shindano hilo ambapo alichukua fomu na baada ya kuzijaza alizirejesha katika ofisi za maliasili wilayani Meatu.

Anasema, wakati akiwa anasubiri matokeo ya fomu hizo, alitembelewa na kundi la viongozi mbalimbali wa ngazi ya wilaya waliofika kukagua eneo lake hilo analoshughulika katika uhifadhi wa mazingira, ambapo walikagua eneo lote na kisha waliondoka wakimtaka asubiri matokeo baada ya kuwa ni mmoja kati ya watu waliojitokeza kushiriki shindano hilo.

“Mbali ya kutembelewa na viongozi hao wa ngazi ya wilaya, lakini pia lilifuata kundi la pili lililokuwa na timu ya viongozi wa ngazi ya mkoa na wao niliwatembeza katika eneo langu lote ambapo waliweza kujionea jinsi ambavyo nimeweza kubuni mbinu mbalimbali katika utunzaji wa mazingira,”

“Baada ya kuondoka kwa timu ya mkoa, muda mfupi likafuata kundi la ngazi ya kitaifa, hawa nao niliwatembeza katika eneo langu lote wakalikagua na wao wakajionea hali halisi ilivyo, na kwa kweli hata hawa nao walipoondoka hawakunieleza jambo lolote juu ya kile walichokiona,” anaeleza Bw. Sambe.

Bw. Sambe anaendelea kueleza, “Alhamisi ya Juni 3, mwaka 2010 nilishangaa kupigiwa simu kutoka ofisi ya mkuu wa wilaya ya Meatu ikinieleza kuwa natakiwa kwenda Dodoma katika kilele cha maadhimisho ya sherehe ya Siku ya mazingira duniani,”

“Sikuamini masikio yangu nilipoelezwa kuwa mimi ni mshindi katika shindano la utunzaji wa mazingira kiwilaya, kimkoa na kitaifa kwa ngazi ya kaya katika utunzaji wa mazingira nchini, na kwamba natakiwa kwenda kukabidhiwa zawadi yangu na Rais Jakaya Kikwete,”

“Nilifurahi sana japo kidogo nilipatwa na wasiwasi, ilibidi nifunge safari ya ghafla kuelekea mkoani Dodoma, nilipofika huko nilikuwa naamini kuwa ni mshindi katika maeneo matatu niliyoelezwa hapo awali,”

“Nilipokea zawadi ya kitaifa ya shilingi milioni mbili na cheti, lakini ilipokuja zamu ya kutangazwa kwa mshindi wa jumla katika maeneo yote yaliyoshindaniwa, nilipatwa na mshituko mwingine baada ya kusikia jina langu likitajwa tena kwa mara ya pili,” anaeleza.

Bw. Sambe anasema alitangazwa kuwa mshindi wa jumla kitaifa wa shindano hilo baada ya kukidhi vigezo muhimu vilivyokuwa vikihitajika ili kumwezesha mtu kutangazwa kuwa mshindi wa jumla, na kwamba moja ya vigezo hivyo ilikuwa ni kuonesha ubunifu wa ziada ambapo katika ushindi huo alipata zawadi ya ngao na shilingi milioni 10.

Anasema kwa upande wake aliweza kuonesha ubunifu wa ziada kutokana na kugundua utengenezaji wa mbolea ya juice ambayo inatengenezwa kutokana na mchanganyiko wa kinyesi cha kuku na sungura, na kwamba mbolea hiyo ilibainika kuwa bora katika kukuzia mimea kuliko mbolea nyingine.

Pia vigezo vingine vilikuwa ni kuwa na choo bora ambapo pia aliweza kuonesha ubunifu wa kutengeneza eneo la kuhifadhia taka ngumu ambazo huwa haziozi na hivyo zikisambaa au kuchomwa huchangia uharibifu wa mazingira kwa kiasi kikubwa.

Anasema amekuwa na utaratibu wa kuwasiliana na watu Halmashauri ya wilaya pale taka hizo zinapojaa wazichukue na kwenda kuzitupa katika maghuba yao badala ya kuzichimbia chini au kuzichoma moto.

Kwa ujumla Bw. Sambe anasema utunzaji wake wa mazingira umeweza kuwasaidia wanakijiji wenzake kuiga mfano wake ambapo mpaka hivi sasa tayari kuna kaya zipatazo 360 ambazo zimeanza kutunza mazingira na kusababisha maeneo yao kupata mvua za uhakika kila mwaka.

Anasema kutokana na mafanikio hayo hivi sasa amekuwa akitoa mafunzo ya utunzaji wa mazingira katika shule saba za msingi wilayani Meatu anazozitaja kuwa ni pamoja na ile ya kijijini kwake Mwambengwa, shule ya msingi Ikigijo, Buhangija, Nkoma, Itaba, Mshikamano, Sapa na Mwanhuzi.

“Suala la uhifadhi wa mazingira ni kitu muhimu sana, pamoja na kwamba nilianza na miti miwili, lakini leo hii eneo langu lina zaidi ya miti 200,000 ya kupanda na mingine ya asili, naamini iwapo jamii ikihamasika katika suala hili!! mazingira yetu yataboreka, maeneo mengi mkoani Shinyanga huko nyuma yaliathirika sana na baadhi yapo katika hatari ya kugeuka jangwa, sasa lazima tubadilike,”

“Binafsi kupitia uhifadhi huu wa mazingira nimeweza kuisadia jamii inayonizunguka kwa kuwapatia matunda ninayovuna katika miti yangu, sina kawaida ya kuuza matunda, ninagawa bure ili kuihamasisha jamii ione umuhimu wa kupanda miti, na pia katika matatizo ya misiba nimekuwa ninasaidia kuni bure,”

“Wito wangu kwa jamii ninawataka wabadili tabia, badala ya kuharibu mazingira sasa wageukie utunzaji wa mazingira ili yawatunze, mimi kupitia kuni na nyasi ninazouza kwa wafugaji kwa mwaka napata zaidi ya shilingi milioni tatu, sasa kama ningeharibu mazingira faida hii nisingeipata,” anaeleza Bw. Sambe.

Mkereketwa huyo wa mazingira anamalizia simulizi yake kwa kuwaomba viongozi wa serikali wampatie ushirikiano zaidi ili aweze kuendeleza ndoto yake hiyo muhimu katika suala zima la utunzaji wa mazingira kwani ni kupitia utunzaji wa mazingira pekee ndipo jamii inapoweza kupata hewa safi ya Oxygen
.